Ndege ya Egypt Air imelazimika kutua kwa dharura kwenye uwanja wa ndege wa Larnarca, Cyprus baada ya Rubani kulazimishwa kufanya hivyo akiwa angani na ni baada ya mtekaji huyo kumtishia kwamba anaweza kuilipua ndege kama asingefanya anachoagizwa.
Anachokitaka abiria huyu mtekaji alietajwa kuwa Seif Eldin Mustafa ni pamoja na kuachiwa huru kwa Wafungwa kadhaa wa kike waliofungwa gerezani huko Misri na mmoja wao anaaminika kuwa mke wake.
Waziri wa mambo ya nje ya Cyprus amesema huyu sio mtekaji wala sio gaidi bali ni mjinga mmoja tu asiejua anachokifanya, na kwamba Magaidi ni vichaa lakini sio wajinga…. huyu ni mjinga.
Mpaka sasa uwanja wa ndege wa Cyprus ilikotua kwa dharura ndege hii ya Egypt Air umefungwa na ripoti ya mwisho ilisema abiria wengine waliokuwemo ndani yake waliruhusiwa kutoka nje ya ndege hiyo na kuchukuliwa na basi la uwanja wa ndege lakini wamebaki watu saba ndani ya ndege wakiwemo abiria watatu, Marubani na Wafanyakazi wa ndege.
Wakati ndege hii inatekwa angani ilikua na abiria 81 ambapo 26 ni raia wa kigeni wakiwemo Wamarekani nane, Wabelgiji, Mfaransa mmoja, Muitaliano, Wagiriki wawili na Msiria mmoja ambapo mtekaji alikua anataka ndege ipelekwe Istanbul Uturuki lakini ikashindikana sababu hakukuwa na mafuta ya kutosha.
Kwenye moja ya masharti ya Mtekaji huyu baada ya ndege kutua, ni kutotaka kuona gari lolote la Polisi karibu na ndege hiyo..
Usalama wa viwanja vya ndege Egypt umekuwa kwenye headlines kwa miezi sasa hivi baada ya ndege ya Urusi kuanguka kwenye jangwa la Sinai na kuua abiria wote 224 na Wafanyakazi waliokuwemo ndani yake baada ya ndege hiyo kuangushwa na bomu ambalo lililokuwemo ndani ya ndege.
Habari zilizotolewa saa tisa alasiri ya Kenya na Maofisa wa Cyprus ni kwamba Mtekaji huyu amekamatwa tayari baada ya jitihada za askari wake kwenye uwanja huohuo wa ndege ikiwa ni saa kadhaa baada ya purukushani kuanzia ndege ilipotekwa.