Friday 18 March 2016

Unknown

BREAKING: MOHAMED ALI WRITES AN OPEN LETTER TO UHURU, NKAISSERY AND MARWA




Unapotaka kufanya maasi anza kwa kuzima sauti za wanyonge, watetezi wao na vyombo vya habari. Kisha kila mwaka ongeza idadi ya polisi na vifaa vya kivita kupasisha ujumbe fulani kuwa mtashinda kwa mabavu pasi na kuheshimu maamuzi ya wapiga kura. Kisha kuwa na viongozi feki watakao pasisha ujumbe huo kwa matamshi yao ya kuwatishia wakenya kuwa wataiba na kununua kura hizo, wengine kusema watatawala hadi mwaka wa 2022 na wengine kuwahadaa viongozi kwa kuwanyang’anya walinzi na bunduki zao walizopewa baada ya kufuata utaratibu wote unaotakiwa na serikali.
Hii ndio sura kamili ya serikali ya Jubilee ambao sasa wanajiita JAP. Katika maeneo ya pwani JAP inajulikana kama jambazi ameingia pwani. Msemo huu ulijitokeza wakati wa kampeni za CORD na KANU Malindi na Kericho mtawalia. Ningelipenda kuchambua kisa cha Malindi na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho. Yanayompata Joho si masuala ya haki ila ni maswala ya kumtafuta mwenye umbwa. Nelson Marwan a Joseph Nkaissery hawafanyi mambo haya yanayoonekana sasa kama ya kitoto na wakenya kwa idhini yao wenyewe. Nelson Marwa na Joseph Nkaissery wanasukumwa na kiongozi aliyejuu. Leo nitawachambua watu watatu kuweka mambo sawa.

UHURU KENYATTA.

Ametajwa na wengi kama Rais wa ziara na mtalii nambari mmoja. Sio matamshi yangu bali ya wakenya mitandaoni. Ameonekana kama Rais asiyeweza chenga wala kupiga kona, butu na anayeogopa kutoa maamuzi ya busara kuendeleza Kenya. Wengi wanasema hakuwa na haja ya Urais ila alikuwa akitaka kujitoa katika minyororo ya mahakama ya jinai huko hague Uholanzi. Ni rais wa ule msemo wa kusema na kuenda kwani unapoona rais anayekubali kuwa ufisadi umo hata ndani ya ofisi yake na hachukui hatua basi jua kuna kasoro kubwa. Wengine wanamtaja kama rais wa burudani, yaani rais wa kupenda anasa na wa kizazi kipya. Haya yote ni matamshi na hisia kutoka kwa baadhi ya wakenya lakini ukweli wa mambo ni kuwa Uhuru Kenyatta anajua yote yanayotendeka humu nchini. Uhuru Kenyatta huenda anachochewa na baadhi ya vitoto vidogo vilivyojawa na ukabila ndani ya ikulu kupasisha jumbe za ki-imla. Uhuru Kenyatta anajua masaibu yote yanayompata Ali Hassan Joho, anajua shida za taifa hili lakini anaonekana kutojali kwa sababu hachukui hatua za dharura kuwanyamazisha wafisadi. Yanayompata Joho hakika Uhuru Kenyatta anayajua na kuyafahamu vyema kama kiongozi wa taifa. Asichojua Uhuru Kenyatta ni kuwa Kenya si ya zamani, Kenya sio Uganda wala Burundi, Wakenya ni wasomi na watu wajanja. Siasa za mimi ndio jogoo zilipitwa na wakati. Uhuru Kenyatta anafaa kujua kuku ni kuku Jogoo ni jina tu. Uhuru Kenyatta afaa ajue wazi kuwa alipowafikisha wakenya tangu na mwaka wa 2013 yamewafika kooni na vyombo vyake vya usalama kutaka kutumia mabavu na dhulma dhidi ya wakenya hakutafua dafu. Wanachojaribu kufanya sasa ni kupima maji pwani ya Kenya. Wakiona wakenya hawafanyi lolote basi wataendeleza sera hizo kwengine hususan katika ngome za CORD. Uhuru Kenyatta wanaokuzunguka hawakuambii ukweli lakini mimi Mohammed Ali nakuweka wazi wazi na kukuambia ndugu yangu umefeli. Umefeli pakubwa na iwapo hutachukua hatua za dharura basi utazidi kuwagawanya wakenya wapenda amani kwa misingi ya kikabila. Uhuru Kenyatta babako alipokuwa Rais hakuwasaidia wana-gatundu wala kabila lake. Wana-gatundu ni maskini wakubwa hadi wa leo lakini kwa sababu ya siasa za kikabila hawaoni lolote baya na hilo. Uhuru Kenyatta fungua macho na ukomboe taifa hili. Usikubali wanaokuzunguka kuendelea kuzalisha chuki miongoni mwa wakenya. Kenya itabadilika!

JOSEPH NKAISSERY.

Wewe kwanza una kesi ya kujibu. Miaka ya nyuma Februari 22 hadi Mei 22 uliongoza OPERESHENI NYUNDO huko Pokot mahala ambapo makumi ya watu waliuawa na kuteswa huku zaidi ya mifugo elfu ishirini ikiachwa kufa kwa kunyimwa chakula. Madai ya watu kubakwa na kupigwa iligonga vichwa vya habari katika tukio hilo lililotajwa kama MAUAJI YA LOTIRIRI. Unadaiwa kufeli kufika mbele ya tume tarehe 23 mwaka wa 2013 na Aprili nane mwaka uo huo. Tume ilipendekeza ufunguliwe mashtaka lakini ajabu ni kuwa anayetakiwa kujibu maswali hayo mazito ndio sasa waziri wa usalama wa ndani. Huu ni ubakaji wa demokrasia lakini yote tunamwachia Mungu. Joseph Nkaissery leo hii unatumia nguvu za bunduki kuwahadaa wakenya pamoja na matamshi yako. Majuzi ilikuwa mimi na Yassin Juma. Leo ni Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho. Polisi wako wamekuwa vipofu wasioona maasi yanayotekelezwa na serikali yako. Mmeshindwa kuwakamata wezi wa mali ya umma na badala yake kuwahangaisha kina yahe. Mmeshindwa kuwashika wezi wa Eurobond, NYS, Chicken Gate miongoni mwa wezi wengine wanaovalia suti na kujifanya bora zaidi ya wakenya wengine. Joseph Nkaissery siasa si mchezo mchafu, uchafu ni mtu mwenyewe. Usiondoke na jina baya, rekebisha na uache kusikiza vitoto vidogo vya mtandao vinavyokupa ushauri wa chochoroni. Kesho utakuwa raia kama wakenya wengine, utadharauliwa kwa yale yote uliofanya ukiwa uongozini, utakuwa kama yatima na kila ukifungua kinywa utanyamazishwa kutokana na uongozi wako feki wa kuabudu miungu yako midogo. Ni mawaidha tu usije ukanuna na kunitumania wanajeshi!

NELSON MARWA.

Leo sina la kukueleza maana hata sijui nianzie wapi. Jifungie chumbani na ujiulize maswali ya mambo unayoyafanya. Ukipata jawabu basi anza kujirekebisha.
Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.
Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu


COURTESY OF:  Official Jicho Pevu with Mohammed Ali

Subscribe to get more videos :

3 comments

Write comments
Unknown
AUTHOR
19 March 2016 at 14:06 delete

Jicho liwe pevu zaidi !

Reply
avatar
Aviv Manu
AUTHOR
19 March 2016 at 17:45 delete

wape vidonge moha....n wakimeza wakitema shauri yao........

Reply
avatar
Unknown
AUTHOR
21 March 2016 at 08:22 delete

Mohamed Ali anafichua kila kitu chao.

Reply
avatar