Gavana wa Mombasa Hassan Joho amewafurusha polisi waliotumwa kutoa ulinzi nyumbani kwake huko Mombasa. Polisi hao hawakuruhisiwa kuingia nyumbani kwake hali iliowalazimu kukesha nje usiku kucha. Hata hivyo msemaji wa serikali Erick Kiraithe anashikilia kauli kuwa ulinzi wa Joho si muhimu ikizingatiwa hitaji la wakenya milioni 49. Anasema hamna haja ya kuingizwa siasa katika swala hilo.
Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho kwa mara nyingine ameshambulia serikali ya Jubilee wakati huu kuhusiana na mzozo wa kuondolewa kwa walinzi wake akisema hana haja ya ulinzi wa serikali akisema mlinzi wake mkuu ni maulana na wananchi anaowatumikia.
Haya yanajiri huku mshirikishi wa eneo la Pwani Nelson Marwa akionya wale wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria katika eneo la Pwani kuzisalimisha bunduki hizo kabla serikali haijachukua hatua dhidi yao.
Hapo jana seneta wa kaunti hiyo Hassan Omar Hassan aliitaka serikali kuchunguza uhalali wa bunduki zinazomilikiwa na Joho na familia yake.