Friday 11 March 2016

Unknown

"KENYA SI YA MAMAKO" ASEMA MOHAMED ALI, Je alikua anamuambia nani?? Soma zaidi hapa.



Naanza kwa kumwambia ndugu yangu Nelson Marwa afahamu kuwa licha ya wakenya kuambiwa na Aden Dualle kuwa pesa si ya mama yetu, yeye pia afaa afahamu kuwa Kenya si ya mamake pekee bali ni ya wakenya wote yeye pia akiwa mmoja wao. Nasema hivi kwa sababu Nelson Marwa amekuwa mwiba kwa wapwani tangu ateuliwe kuwa kamishna wa kaunti ya Mombasa na sasa afisa mkuu wa polisi pwani nzima. Nelson Marwa ni mtu wa maajabu na historia yake inaonyesha wazi kuwa Marwa ni mtu anayeishi maisha ya ki-siri na mtu anayetajwa kujitenga na watu wengine. Ni vigumu kujua maisha ya Nelson Marwa maana wengi hawajui bibi au watoto wake. Ni mtu msiri mno, mtu anayedaiwa kukataa ulinzi na jumba alilopewa na serikali kwa madai ya kuhofia maisha yake. Anadaiwa hata kumkataa afisa wa polisi msomali kumlinda kwa kuwa na fikra za kudhania atashambuliwa na afisa huyo msomali. Haya ni madai ninayopewa na wandani wangu katika afisi yake ingawa hatuwezi bainisha.
Nelson Marwa anadaiwa kupiga kambi katika hoteli ya Ocean Breeze iliyopo hapo Tudor, hoteli anayodaiwa kuimiliki katika kipindi kifupi huko Mombasa. Ni katika hoteli hii ndipo sura za watu wa Jubilee pamoja na Mbunge wa Nyali Hezron Awiti bollo hudaiwa kukutana na kujadili siasa za Kenya na jinsi ya kuwasukuma ukutani wafuasi wa upinzani. Nelson Marwa mara kwa mara ameonekana kama kibaraka wa Jubilee na wala sio afisa chapa kazi anayetaka kuwahudumia wakenya. Nelson Marwa huenda akaingia kwenye vitabu vya wale maskauti 36 wanaoropokwa kila kukicha pasi na ushahidi wowote. Kila mara anapofungua kinywa chake lake kuu limekuwa kukashifu mambo asiyokuwa na ushahidi nayo na kutishia raia wapenda amani kwa mtutu wa bunduki kama alivyonakiliwa miaka ya nyuma akisema kuwa polisi wawaue kwa kuwapiga risasi mtu yeyote atakayepatikana na bunduki au kuwa mshukiwa wa kundi lolote haramu. Katika uchaguzi mdogo wa Malindi Nelson Marwa amewaonyesha wakenya sura yake aliyokuwa akiificha kwa miaka na mikaka. Marwa alijaribu kugeuza malindi kuwa Uganda ndogo kwa kutumia maafisa wake wa polisi pamoja na wanajeshi walioonekana kupiga kambi malindi na magari yao ya kutisha kuwahadaa wana ODM kwa kuwashika kiholela na kuwafungia kilifi badala ya Malindi. Wachache waliokamatwa wa Jubilee wakiwa wamejaza pesa za hongo mfukoni walichukuliwa tu kama wasamaria wema na kuachiliwa mara moja badala ya kufikishwa mahakamani kama wale wa upinzani. Kama nimekosea mnikosoe lakini hofu yangu ni kwamba Nelson Marwa anatumiwa kama daraja la kuvuruga haki ya wapwani kutoa maamuzi yao mwaka wa 2017 kwa sababu pwani ni ngome kuu ya upinzani.
 Nelson Marwa tayari ameanza alfu lela ulela ya kuwepo kwa MRC na vikundi vingine ikikumbukwa wazi kuwa tangu Uhuru Kenyatta kuapishwa suala la MRC lilitokomea katika kaburi la sahau. Lakini sasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao Nelson Marwa ameanza tena vihoja vyake vya kutoa misukosuko pwani. Mabadiliko ya hivi majuzi ya polisi pia ni ya kutia shauku kwani idadi ya maafisa wakuu waliopelekwa pwani ya Kenya wana husishwa na dhulma za tangu na jadi na huenda uhamisho huu ukawa kama mojawapo ya njia ya serikali kujiandaa kulemaza kura za upinzani pwani ya Kenya. Sio pwani tu bali maeneo kama ya kaskazini kusini, nyanza na magharibi mwa Kenya mchezo huu umeanza kupangwa kimya kimya. Duru zinaniarifu kuwa Robert Kitur rafiki wa Nelson Marwa enzi zake Mombasa huenda akahamishwa hadi Nairobi kuafikisha malengo ya uchaguzi mkuu ujao Nairobi na viunga vyake. Kwa ufupi sisemi Nelson Marwa ni mtu mbaya, la hasha nasema tu Nelson Marwa kama mtumishi wa umma na afisa mkuu wa polisi anafaa ajiepushe na siasa chafu za kutumiwa na walio mamlakani kwa maslahi yao binafsi. Nelson Marwa anafaa akumbuke kuwa tuliwaona waliokuwa wakijifananisha na simba na kuogopewa na wengi kama marehemu inspekta mkuu Timothy Kamunde aliyeogopewa na wengi enzi za flying squad, Zabed Maina aliyeuawa na afisa mwenzake huko kitui miongoni mwa maafisa wengine waliotumika vibaya na serikali zilizokuwa mamlakani. Enyi baadhi ya maafisa wakabila na wafisadi ninawakumbusha kuwa Kenya ni kubwa kushinda miungu yenu midogo, Kenya ni kubwa kushinda hizo senti mnazopewa zisizokuwa na adabu. Nawaomba na kuwasihi msiingilie siasa na kubaka haki ya msingi ya wakenya mwaka wa 2017. Nawasihi mheshimu maamuzi ya wakenya. Nawasihi mjiepushe kuchoma taifa hili kwa shilingi mbili mnazopewa kuwadhulumu wakenya na sauti zao. Komeni kuwapigia wakenya kura bila maamuzi yao, komeni kuzua propaganda za kuwahofisha wakenya ili wasiweze piga kura.
Bwana Nelson Marwa kama hakukuwa na MRC mwaka wa 2013 Uhuru Kenyatta alipoapishwa basi hamna MRC mwaka wa 2017. Hizi ni propaganda fiche na hila fiche dhidi ya ngome za upinzani. Siandiki haya kuunga mkono chama Fulani bali naandika haya kuwataka mjue kuwa wakenya si wajinga, wakenya wamekomaa na wanajua hadithi zenu za longo longo na daganya toto jinga. Safari hii hamna watoto wa kudanganya. Itabidi mjidanganye wenyewe kwa kukubali kuwa nguvu za wengi haziwezi zimwa na sauti ya watu wawili wanaotaka kutumia mtutu wa bunduki kuwanyamazisha. Hii ni Kenya mpya na wakenya wanaamini watashinda hata serikali ikijaribu kuiga tabia za Uganda na kutaka kutawala kwa nguvu. Wakenya bado hawajapata ukombozi wanayotaka na kukamia kila kukicha. Ushindi wa mwaka wa 2017 utakuwa ushindi wa Eurobond, Nys, Chicken Gate, SGR na ukombozi wa pili tangu mwaka wa 1963. Huu utakuwa ushindi wa wakenya dhidi ya wezi wachache walio madarakani na wanaotaka kutawala Kenya kwa mabavu. Ushindi wa wakenya dhidi ya idara za ki-usalama zinazowadhulumu wakenya na zilizojaa ukabila, ushindi dhidi ya magaidi waliovalia suti na wanaofyonza damu ya wanyonge kila kukicha. Ashakum si matusi na kama nimekuudhi nasema pole. Mungu ibariki Kenya.
Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.
Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

Subscribe to get more videos :